IEBC yakosolewa kwa kutishia kuahirisha uchaguzi mdogo wa Ol Kalou

Ushindani mkali umeibuka kati ya mgombea wa UDA Muchina Nyagah na Sammy Ngotho wa DCP kuelekea uchaguzi mdogo wa Julai 16.

Martin Mwanje
2 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Tishio la Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Erastus Ethekon kuahirisha uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ikiwa tume hiyo itabaini mazingira ya kuandaa uchaguzi huo si salama limekosolewa vikali. 

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou umepangwa kufanyika Alhamisi wiki ijayo.

“Ikiwa, kwa kufanya kazi na maafisa wa usalama na washikadau wengine, tutabaini kuwa mazingira si salama sana ili kuandaa uchaguzi mdogo huko Ol Kalou, hatutakuwa na budi ila kuchukua hatua ambayo si nzuri na kali zaidi ya kuahirisha uchaguzi huko Ol Kalou,” alitishia Ethekon hiyo jana wakati akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Usuluhishaji Migogoro ya Kabla ya Uchaguzi jijini Nairobi.

Miongoni mwa wanaokosoa hatua hiyo ni Naibu Rais wa zamani na kiongozi wa chama cha DCP Rigathi Gachagua.

Gachagua, akizungumza leo Ijumaa jijini Nairobi, alishangaa ni kwa nini IEBC haikuahirisha chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Malava, Narok na Kasipul Kabondo licha ya vurugu alizodai zilikithiri katika maeneo hayo wakati wa chaguzi hizo.

“Sasa unatumiwa na Rais Ruto kutaka kuahirisha uchaguzi huo kwa sababu anafahamu atashindwa vibaya,” alidai Gachagua.

Si yeye tu aliyepinga kuarishwa kwa uchaguzi huo.

Viongozi wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wakiongozwa na mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri pia walikosoa vikali hatua hiyo.

Wameitaka IEBC kuhakikisha uadilifu kwenye mchakato wa uchaguzi badala ya kuibua mashaka yasiyokuwa na msingi wakati kampeni zikiingia mkondo wa lala salama.

Chama cha Jubilee pia kimepinga vikali kuahirishwa kwa uchaguzi huo.

Ushindani mkali umeibuka kati ya mgombea wa UDA Muchina Nyagah na Sammy Ngotho wa DCP huku ukitumiwa kama kipima joto cha ubabe wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

 

Share This Article