IEBC yatema cheche uchaguzi mdogo wa Ol Kalou

Uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ol Kalou utaandaliwa Julai 16 huku ushindani mkali ukiibuka kati ya Muchina Nyagah wa UDA na Sammy Ngotho wa DCP. 

Martin Mwanje
2 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetoa kali dhidi ya ukiukaji wa kanuni yake ya maadili kuelekea uchaguzi mdogo uliopangwa kuandaliwa Julai 16 mwaka huu. 

Mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon ametishia kuwazuia wagombea watakaokiuka kanuni hiyo na hata kufutilia mbali uchaguzi huo ikiwa mazingira ya usalama yatakuwa mabovu.

“Ikiwa kanuni hiyo itakiukwa, hatua zifaazo zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuia baadhi ya wagombea hao, ikiwa si wote, wale wanaohusika,” alionya Ethekon.

“Ikiwa, kwa kufanya kazi na maafisa wa usalama na washikadau wengine, tutabaini kuwa mazingira si salama sana ili kuandaa uchaguzi mdogo huko Ol Kalou, hatutakuwa na budi ila kuchukua hatua ambayo si nzuri na kali zaidi ya kuahirisha uchaguzi huko Ol Kalou.”

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo leo Alhamisi wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Usuluhishaji Migogoro ya Kabla ya Uchaguzi uliofanyika jijini Nairobi.

Kauli zake zinakuja wakati ambapo kumekuwa na madai ya kuwahonga wapiga kura, kufanya kampeni nyakati za usiku, vurugu na utoaji wa taarifa za upotoshaji katika eneo bunge la Ol Kalou.

Baadhi ya maafisa wa serikali pia wamenyoshewa kidole cha lawama kwa kumfanyia kampeni mgombea wa chama cha UDA Muchina Nyagah.

Nyagah anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha DCP Sammy Ngotho.

Uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ol Kalou utaandaliwa Julai 16 kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho wakati akitibiwa katika hospitali moja jijini Nairobi mwezi Machi mwaka huu.

Share This Article