EACC kurejesha fidia ya ardhi ya Ruaraka

Itawafungulia mashtaka ya jinai wanaohusishwa na sakata tata ya fidia ya ardhi hiyo ya umma

Marion Bosire
2 Min Read
Abdi A. Mohamud, Afisa Mkuu Mtendaji EACC

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC imetangaza mipango ya kurejesha shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa kama fidia kwa ardhi ya umma huko Ruaraka.

Katika taarifa, tume hiyo imetabgaza kwamba itawafungulia mashtaka ya jinai watu wanaohusishwa na sakata tata ya fidia ya ardhi hiyo ya umma kufuatia uamuzi muhimu wa Mahakama ya Rufaa.

Mahakama ya Rufaa ilithibitisha uamuzi wa awali wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi uliotangaza kuwa fidia iliyolipwa kwa ardhi inayokaliwa na Shule ya Sekondari ya Ruaraka na Shule ya Msingi ya Drive Inn ilikuwa kinyume cha sheria, batili na isiyo na nguvu za kisheria.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Abdi A. Mohamud, uchunguzi ulibaini kuwa kipande hicho cha ardhi cha ekari 13.5 kilikabidhiwa Serikali bila malipo kama sharti la kugawanywa kwa ardhi ya awali, na hivyo kuwa mali ya umma.

Tume hiyo ilisema ilifanikiwa kupata hati miliki ya awali ya ardhi hiyo na kuweka zuio la kisheria ili kulinda maslahi ya umma baada ya malipo hayo yenye utata kufanyika.

Kufuatia uamuzi wa mahakama, EACC itaanza mchakato wa kurejesha shilingi bilioni 1.5 zilizolipwa kwa kampuni za Afrison Export Import Limited na Huelands Limited kupitia Whispering Palms Estate Limited chini ya kile ilichokitaja kuwa mpango wa ulaghai wa fidia.

Tume hiyo pia imesema uchunguzi kuhusu nafasi ya maafisa wa umma na watu wengine waliohusika katika mchakato huo umekamilika, na faili itawasilishwa tena kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP kwa hatua zaidi.

Aidha, EACC imezitaka Wizara ya Elimu na Tume ya Taifa ya Ardhi kuharakisha mchakato wa utoaji wa hati miliki za ardhi kwa shule hizo mbili ili kulinda matumizi ya ardhi hiyo kwa manufaa ya umma.

Share This Article