Mmoja kati ya majirani Ureno na Uhispania atafuzu kwa robo fainali na mwingine kurejeshwa nyumbani wakati miamba hao watakapomenyana Jumatatu usiku katika raundi ya 16 ya Kombe la Dunia uwanjani Dallas, Marekani.
Itakuwa mechi ya tatu kwa mibabe hao kukutana katika Kombe la Dunia baada ya Uhispania kuwashinda Wareno bao moja kwa bila mwaka 2010 katika raundi ya 16, kabla ya kuchuana tena katika hatua ya makundi mwaka 2018, mechi iliyomalizikia sare ya 3-3.
Kwa jumla, Ureno na Uhispania watakuwa wakipambana Jumatatu usiku kwa mara ya 12, Uhispania wakishinda mechi 5 na 6 kumalizikia sare.
Ureno iliwashinda Uhispania kwa penalti 5-3 kwenye fainali ya UEFA Nations League mwaka 2025.
Timu zote zinajivunia kutopoteza mechi kwenye fainali za mwaka huu, Ureno ikimaliza ya pili kundini K kwa alama 5 baada ya kutoka sare na DRC na Colombia na kuishinda Uzbekistan na hatimaye kuwabwaga Croatia 2-1 katika raundi ya 32.
Uhispania waliongoza kundi H kwa pointi 7, wakitoka sare ya Cape Verde kabla ya kuwashinda Saudi Arabia na Uruguay na hatimaye kuwalemea Austria 3-0 katika raundi ya 32.
Mechi hiyo itarushwa mubashara na runinga ya KBC Channel 1.