Nyota Ndogo awasili Dar maadhimisho ya Bongo Flava

Atatumbuiza katika sherehe ya miaka 30 ya Bongo Flava Ijumaa, Julai 10, 2026, katika ukumbi wa mlimani City.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa Kenya Mwanaisha Abdalla ambaye wengi wanamfahamu kama Nyota dogo, yuko jijini Dar nchini Tanzania kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 30 ya uziki wa Bongo Flava.

Nyota Ndogo aliwasili jana jioni jijini Dar es Salaam ambapo alilakiwa katika uwanja wa ndege na waandalizi na kisha kuhojiwa na wanahabari.

Aliwaonjesha wimbo wake maarufu wa ‘Watu na Viatu’ na kusema kwamba zamani kulikuwa na umoja kati ya wasanii wa Kenya na wale wa Tanzania na anaamini ndiyo sababu ya kualikwa kwake.

Awali kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii huyo alitangaza kwamba atakuwa mmoja wa watumbuizaji katika sherehe hiyo ya miaka 30 ya Bongo Flava tarehe 10 mwezi huu katika ukumbi wa mlimani City.

Leo asubuhi mwimbaji huyo amehojiwa na watangazaji Irene Kilenga, Kipande, Godwin Mawanja, Mutente na Fatma Likwata katika kipindi cha ‘Joto la Asubuhi’ kwenye kituo cha redio cha E Fm.

Msanii mwingine wa Kenya atakayehusika katika maadhimisho hayo ni Paul Julius Nunda almaarufu Jua Cali. Mwanzilishi huyo wa mtindo wa Genge alichapisha video kwenye Instagram inayomwonyesha akitangaza hilo.

Msanii wa muziki Mdee Ali, ndiye anaandaa tamasha hiyo ambayo inatarajiwa kukutanisha wasanii wakongwe wa Bongo Fleva na kusherehekea mchango wa muziki huo katika jamii.

Baada ya hafla hiyo Ijumaa wahusika wa maadhimisho hayo wanatarajiwa kuyapeleka katika mikoa mbali mbali, pendekezo ambalo tayari Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda ameridhia.

Matonya au ukipenda Seif Shaaban ambaye alikuwa nchini Kenya na ambaye ni mmoja wa wasanii wakongwe wa Bongo Flava, naye amewasili Dar es Salaam kwa ajili ya tamasha hiyo muhimu.

Share This Article