Uingereza yajituma kibabe na kuwabandua wenyeji Mexico

Uingereza walifanikiwa kulinda lango lao na kusajili ushindi wa 3-2, na sasa watakabiliana na Norway Julai 11 katika kwota fainali.

Dismas Otuke
1 Min Read

Uingereza walikabiliwa na upinzani mkali kabla ya kuwabandua wenyeji Mexico mabao 3-2 na kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia mapema Jumatatu katika uwanja wa Azteca.

Jude Bellingham alipachika mabao mawili katika dakika za 36 na 38, naye Julian Quinones akakomboa moja kwa wenyeji na kipindi cha kwanza kumalizikia kwa uongozi wa Three Lions  wa 2-1.

Kipindi cha pili, Uingereza walijipata taabani baada ya beki Quansah kulishwa kadi nyekundu katika dakika ya 54 kwa kumchezea ngware Jesus Gallardo.

Dakika chache baadaye, mlinda lango wa  Mexico Raul Rangel alimwangusha  wing’a wa Uingereza Anthony Gordon katika eneo la penalti na kuwazawadi tuta lililopachikwa kimiani na Harry Kane dakika ya 60, likiwa bao lake la sita katika fainali za mwaka huu.

Nahodha Kane pia alimwangusha Brian Gutierrez katika kijisanduku na kuwapa Mexico penalti iliyounganishwa na Raul Jimenez dakika ya 69.

Licha ya kujituma na kusukumwa na mashabiki wa nyumbani, Uingereza walifanikiwa kulinda lango lao na kusajili ushindi wa 3-2.

Sasa watakabiliana na Norway Julai 11 mjini Miami nchini Marekani katika kwota fainali.

Share This Article