Waokoaji mjini Kyiv wanaendeleza juhudi za kutafuta watu waliokwama chini ya vifusi vya majengo ya makazi yaliyoharibiwa, katika duru ya pili ya mashambulizi ya Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine
Watu wasiopungua tisa wanaripotiwa kuuawa kwenye mashambulizi hayo ndani ya kipindi cha wiki moja.
Msimamizi mkuu wa masuala ya kijeshi wa Kyiv, Timur Tkachenko, amesema watu 46 walijeruhiwa, wakiwemo watoto wasiopungua watano.
Mashambulizi hayo yamefanyika wakati wa mkutano wa kilele wa NATO nchini Uturuki, ambako Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump.
Saa chache kabla ya mashambulizi hayo ya hivi karibuni, Zelensky alionya kuwa Moscow ilikuwa ikijiandaa kufanya shambulio jingine kubwa dhidi ya Kyiv, kufuatia mashambulizi ya Alhamisi yaliyosababisha vifo vya watu 30.
Kwa mujibu wa Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, makombora ya Urusi yalipiga majengo kadhaa kote jijini humo na kusababisha milipuko ya moto katika baadhi ya majengo ya makazi.
Maghala na karakana moja ya magari pia viliharibiwa.
Picha kutoka Kyiv zinaonyesha vifusi vinavyoteketea na magari yaliyoungua yaliyotapakaa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo. Video pia zinaonyesha vikosi vya uokoaji vikiendelea kuchunguza vifusi Jumatatu asubuhi kutafuta manusura.
Zelensky alisema Jumapili, saa chache kabla ya mashambulizi hayo, kwamba taarifa za kijasusi zilionyesha Kyiv ingekumbwa na wimbi la pili la mashambulizi ya Urusi ndani ya wiki moja.
Baada ya mashambulizi makali ya ndege zisizo na rubani na makombora usiku wa Alhamisi kuelekea Ijumaa, makumi ya maelfu ya wakazi walikimbilia vituo vya treni za chini ya ardhi huku ving’ora vya tahadhari vikilia mapema Ijumaa asubuhi.
Ukraine imeishutumu Moscow kwa kulenga makusudi maeneo ya raia katika shambulizi hilo lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 30.
Hata hivyo, Urusi imesema ililenga vituo vya kijeshi na miundombinu ya nishati kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Ukraine dhidi ya vituo vya umeme na miundombinu ya nishati ndani ya eneo la Urusi.
Mashambulizi hayo yaliendelea usiku kucha, huku umeme ukikatika kwa muda katika mji wa Sevastopol ulioko Crimea, eneo linalodhibitiwa na Urusi.
Kabla ya mkutano wa NATO, Zelensky aliwataka washirika wa Ukraine kutochelewesha utoaji wa makombora ya masafa marefu yatakayotumika dhidi ya Urusi.
Akiandika kupitia mtandao wa X, Zelensky alisema: “Kucheleweshwa kwa makombora ya ulinzi wa anga… kunamaanisha kupotea kwa maisha ya watu na kunaihamasisha Urusi kuendeleza vita.”
Zelensky pia ameiomba Marekani kuipa Ukraine leseni ya kutengeneza makombora ya ulinzi.