Misri, Ghana na Cape Verde wabeba matumaini ya Afrika leo

Black Stars chini ya uongozi wa Carlos Queiroz,wanawania kufuzu kwa raundi ya 16 bora kwa mara ya pili tangu mwaka 2010.

Dismas Otuke
3 Min Read

Misri maarufu The Pharaohs, Black Stars kutoka Ghana na Blue Sharks kutoka Cape Verde, watarejea uwanjani Ijumaa usiku na mapema Jumamosi wakibeba matumaini ya bara la Afrika katika fainali za Kombe la Dunia.

Misri wakiongozwa na Mohamed Salah watakabiliana na Australia Ijumaa, saa tatu usiku katika uwanja wa Dalllas, Marekani.

Socceroos ya Australia wanacheza kwa mechi ya mwondoano kwa mara ya tatu na watakuwa wakiwinda ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mwaka 2006 na 2022 kwa mabingwa Italia na Argentina mtawalia.

Australia, wanaoorodheshwa nafasi ya 27 duniani, waliishinda Uturuki mabao 2-0, wakapoteza kwa Marekani kwa idadi sawa ya mabao na kutoka sare tasa na Paraguay na kumaliza nafasi ya pili kundini D.

Misri wanaoshiriki mwondoano kwa mara ya kwanza wanashikilia nafasi ya 29 duniani na walimaliza nafasi ya pili kundini G kwa alama 5, wakitoka sare ya 1-1 na Ubelgiji, wakailemea New Zealand 3-1 na kutoka sare ya 1-1 na Iran.

Saa saba usiku itakuwa zamu ya limbukeni Cape Verde ukipenda Blue Sharks kumenyana na mabingwa watetezi Argentina uwanjani Miami, Marekani.

Cape Verde iliyo ya 67 ulimwenguni, ilimaliza ya pili katika kundi H kwa alama 3, ikitoka sare tasa na Uhispania, ikaambulia sare ya 2-2 dhidi Uruguay na kutoka sare kappa dhidi ya Saudi Arabia.

Upande wao Argentina wanaoongoza msimamo wa dunia walichukua nafasi ya kwanza katika kundi J, wakizo alama 9, wakiipiga Algeria 3-0, wakailemea Austria 2-0 na kuilaza Jordan 3-1.

Hatimaye saa kumi unusu alfajiri Jumamosi, mabingwa mara nne wa Afrika Ghana watamenyana na Colombia katika mechi ya mwisho ya raundi ya 32 kiwarani Kansas City.

Colombia ni ya 13 duniani na waliongoza kundi K kwa alama 7, wakisajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Uzbekistan na 1-0 dhidi ya DRC kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Ureno.

Los Cafetoros ya Colombia wanajivunia kutopoteza mechi dhidi ya mpinzani wa Afrika na watalenga kufuzu kwa raundi ya 16 kwa mara ya tatu mtawalia.

Ghana ilizoa alama nne na kumaliza ya tatu kundini K, wakiishinda Panama bao moja kwa bila kabla ya kwenda sare tasa na Uingereza, lakini wakashindwa 2-1 na Croatia.

Black Stars chini ya uongozi wa Carlos Queiroz wanawania kufuzu kwa raundi ya 16 bora kwa mara ya pili tangu mwaka 2010.

Share This Article