Rais William Ruto leo Alhamisi amekagua ujenzi wa Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Bomas, akisema utakapokamilika utaboresha uwezo wa Nairobi wa kuwa kitovu cha mikutano kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, kiongozi wa taifa alisema jumba hilo pia litafanikisha kuongeza idadi ya watalii hadi zaidi ya wageni milioni tano na mapato ya zaidi ya shilingi trilioni 1 kufikia mwaka 2028.
“Nimeridhishwa na hatua zilizopigwa kwenye ujenzi wa Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Bomas (BICC),” alisema Rais Ruto.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto pia aliongoza mkutano ulioshughulikia baadhi ya changamoto zilizopo ili kuharakisha ujenzi huo ikiwa ni pamoja na miundombinu imara ya nguvu za umeme kupiga jeki shughuli za mikutano.