Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga ameidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya wanafunzi waliohusishwa na mkasa wa moto katika shule ya wasichana ya Utumishi, kaunti ya Nakuru, ambapo wanafunzi 16 walifariki na zaidi ya 70 kujeruhiwa.
Kwenye taarifa, Ingonga alisema ofisi yake imechunguza kwa makini ripoti iliyowasilishwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusiana na kisa hicho kilichotokea Mei 28, 2026.
Kulingana na DPP, washukiwa 9 ambao wanazuiliwa, watakabiliwa na mashtaka 16 ya mauaji ya wanafunzi waliofariki kwenye mkasa huo.
“Baada ya kuchunguza ushahidi uliowasilishwa, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ameidhinisha mashtaka dhidi ya wanafunzi wanaoshukiwa. Washukiwa hao watakabiliwa na mashtaka 16 ya mauaji kutokana na mkasa huo,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, DPP alielezea wasiwasi kuhusiana na idadi ya mashambulizi ya moto na uhalifu mwingine kwenye taasisi za elimu kote nchini, akionya kuwa wale watakaopatikana watakabiliwa vikali kisheria.
Aidha, alizifariji familia, marafiki na jamii nzima ya shule hiyo kufuatia vifo vya wanafunzi hao 16.
“Afisi hii imejitolea kuhakikisha haki inapatikana kupitia mchakato wenye usawa, usioegemea upande wowote na unaozingatia ushahidi,” aliongeza Ingonga.
Wanafunzi 9 wanaozuiwa rumande kuhusiana na mkasa huo, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Juni 24, 2026.