Kenya na Japani zimetia saini mkataba wa kifedha wa shilingi bilioni 22.1 unaolenga kuchochea ukuaji wa sekta ya utengenezaji wa magari nchini Kenya.
Mpango huo utatekelezwa na kampuni ya Japani ya Nippon Export and Investment Insurance (NEXI).
Rais William Ruto amesema kuwa mkataba huo ni matokeo ya moja kwa moja ya ziara yake ya kiserikali nchini Japani mwaka 2024 na ushiriki wa Kenya kwenye Kongamano la Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) jijini Tokyo mwaka 2025.
“Tunapoendelea kupanua vyanzo vya ufadhili wetu, tunaendelea kujenga ushirikiano na mataifa yanayotoa fursa sawa, kwa misingi ya kuheshimiana na ufanisi wa pamoja,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto aliyasema hayo Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi, aliposhuhudia hafla ya kutiwa saini kwa mkataba huo kati ya serikali ya Kenya na kampuni ya NEXI iliyowakilishwa na Afisa Mkuu Mtendaji Atsuo Kuroda.
Ruto alisema Kenya itatumia teknolojia na tajiriba ya muda mrefu ya Japani katika sekta ya viwanda ili kupanua uwezo wa taifa hili wa utenegenezaji bidhaa na kuwa na magari mengi yaliyotenegenezewa hapa nchini.