Misri maarufu kama Pharaohs walitoka nyuma na kusajili ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya New Zealand katika mechi ya pili ya kundi G kuwania Kombe la Dunia iliyochezwa mapema Jumatatu mjini Vancouver, Canada.
Finn Surman aliwaweka New Zealand kifua mbele kunako dakika ya 15 na kuongoza hadi kuelekea mapumzikoni.
Mostafa Ziko aliwarejesha Misri mchezoni kwa bao la dakika ya 58 kabla ya kumwandalia pasi Mohammed Salah aliyewaweka uongozini dakika tisa baadaye.
Salah pia alitoa pasi kwa Trezeguet dakika nane kabla ya kipenga cha mwisho na kupata ushindi wa 3-1, unaowaweka kileleni pa kundi hilo kwa alama 4.
Ushindi huo ni wa kwanza katika historia ya Misri katika Kombe la Dunia.
Ubelgiji na Iran wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 2 kila moja huku New Zealand ikishika nanga kwa alama moja.