Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah afanya ziara rasmi Tanzania

Tanzania na Namibia zimedumisha uhusiano mwema wa kidiplomasia, tangu Namibia ilipopata uhuru wake mwaka 1990.

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais wa Namibia Dr. Netumbo Nandi-Ndaitwah afanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Tanzania.

Rais wa Namibia Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, inayolenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Ziara hiyo ya Dkt. Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania, inadhamiria kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya biashara, uwekezaji, usalama wa kikanda na ubadilishanaji wa utamaduni.

Aidha, ziara hiyo inajiri wakati ambapo nchi hizo mbili zinalenga kupanua chumi na mitandao ya kibiashara licha ya kwamba ni washirika wa jadi.

Tanzania na Namibia zimedumisha uhusiano mwema wa kidiplomasia, tangu Namibia ilipopata uhuru wake mwaka 1990.

Huku ikijivunia bandari ya bahari hindi na idadi ya watu zaidi ya milioni 60, Tanzania ina fursa nzuri ya soko la bidhaa kutoka Namibia, huku taifa hilo la kusini mwa Afrika likijivunia madini kama vile shaba na Urani miongoni mwa mengine, na ambayo yanawavutia wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania.

Share This Article