Maafisa wa Polisi nchini Uganda wamewakamata washukiwa 13 wanaodaiwa kuwa wanachama wa mtandao unaohusika na wizi wa pikipiki.
Kwenye operesheni ya kijasusi, maafisa hao pia walipata pikipiki 44 zinazoaminika kuwa zimeibwa.
Idara ya Polisi nchini Uganda kupitia ukurasa wa X, ilisema operesheni hiyo ilitekelezwa katika eneo la Nakati, wakilishi Wadi ya Nabbingo, wilaya ya Wakiso.
“Operesheni hiyo ilitekelezwa baada ya polisi kupokea habari kwamba eneo moja la kuunda magari, hushughulikia pia pikipiki ambazo ni za wizi, kuziunda upya, kupaka rangi na kuziweka nambari bandia za usajili kabla ya kuzirejesha barabarani tena,” ilisema idara ya polisi.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika korokoro za polisi, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Kulingana na polisi juhudi zinaendelea kuwatafuta wamiliki halisi wa pikipiki hizo, wakitoa wito kwa wananchi waliopoteza pikipiki kujitokeza kusaidia kutambua pikipiki zao.