Chama cha ODM hakikumpa Edwin Sifuna fursa ya kujitetea kabla ya kumvua wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Uamuzi huo umetolewa leo alasiri na Jopo la Utatuzi wa Migogoro ya Kisiasa.
Sifuna ambaye pia ni Seneta wa Nairobi aliwasilisha kesi kwa jopo hilo baada ya kuvuliwa wadhifa huo mwezi Februari mwaka huu, na mahali pake kuchukuliwa na Mwakilishi wa Wanawake wa Busia Catherine Omanyo.
Nao uamuzi wa kumvua Sifuna wadhifa huo uliafikiwa wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la ODM, NEC ulioongozwa na kaimu kinara wa chama hicho wakati huo, Dkt. Oburu Oginga.
Kwenye uamuzi wake, jopo hilo linaloongozwa na Gad Gathu lilitoa uamuzi kuwa si tu kwamba Sifuna hakupewa fursa ya kujitetea, bali hapakuwa na ushahidi kuwa aliarifiwa mienendo yake ingejadiliwa wakati wa mkutano wa NEC.
Uamuzi huo kimsingi una maana kwamba Sifuna ataendelea kuhudumu kama Katibu Mkuu wa ODM, na ikiwa chama hicho bado kina ndoto ya kumpiga kalamu, basi ni lazima kianze upya mchakato wa kumtimua.
Chama cha ODM kimegawanyika katika mirengo miwili, mmoja wa Linda Ground unaoongozwa na Dkt. Oginga huku ule wa Linda Mwananchi ukiongozwa na Sifuna.
Awali, Sifuna alinukuliwa akisema hawezi akahudumu kama Katibu Mkuu wa ODM chini ya uongozi wa Dkt. Oginga ambaye pia ni Seneta wa Siaya.
Huku mizozo kati ya pande hizo mbili ikirindima, itafurahisha kuona namna pande hizo zitakavyopimana nguvu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 pasipokuwepo aliyekuwa kinara wa chama hicho, Hayati Raila Odinga.