Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir amekanusha madai kuwa zabuni ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA imetolewa kwa kampuni fulani kisiri.
Waziri Chirchir pia amekana kuhusika kwa mfanyabiashara Wicknell Chivayo kutoka Zimbabwe kwenye mradi huo, akiongeza kuwa wamepata kufahamu juu ya mfanyabiashara huyo kupitia ripoti za mitandao ya kijamii.
Chirchir akisikitikia madai hayo akisema kampuni zote mbili zilizodaiwa kupewa zabuni hiyo hazikutuma maombi ya kazi hiyo wala gharama ya upanuzi huo siyo shilingi bilioni 375 kama ilivyodaiwa.
“Kampuni zilizotajwa katika ripoti za vyombo vya habari hazikutuma maombi na si sehemu ya wanakandarasi waliowasilisha maombi,” alisema Chirchir wakati madai ya mkataba wa upanuzi wa JKIA kuzingirwa na usiri mkubwa yakitanda.
“Mradi huu unakadiriwa kugharimu takriban shilingi bilioni 154 na wala siyo bilioni 375 kama ilivyodaiwa katika vyombo vya habari.”
Kulingana na Waziri, kampuni mbili zilizotuma maombi ya upanuzi wa JKIA ni China Road and Bridge Corporation (CRBC) na Sinohdro na kwamba mchakato wa kutoa zabuni utamalizika wiki ijayo.
Si mara ya kwanza mkataba wa upanuzi wa uwanja wa JKIA kuzingirwa na utata.
Mwishoni mwa mwaka 2024, mkataba uliotolewa kwa kampuni ya Adani ulifutiliwa mbali baada ya kushamiri kwa madai kwamba ulighubikwa na usiri mkubwa wakati wengi wakitilia shaka jinsi kampuni hiyo ilivyokabidhiwa zabuni hiyo.
Upanuzi wa uwanja wa JKIA umepangiwa kuanza wakati wowote mwaka huu.