Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamewakamata washukiwa watatu zaidi wanaohusishwa na uvamizi katika kanisa la All Saints Cathedral Jijini Nairobi, na kuvuruga mkutano uliokuwa ukiendelea.
Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao waliwatafuta na kuwakamata washukiwa hao George Omondi Otieno, Effenburg Wanyama Khisa, na Melvin Alumasa Bwani katika maeneo tofauti ya Nairobi.
Kwenye operesheni hiyo, maafisa hao pia walipata pikipiki yenye nambari za usajili KMFH 161S, inayoaminika kutumika kwenye uvamizi huo.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema ilipata simu kadhaa za mkononi kutoka kwa washukiwa hao na zitatumika kwenye uchunguzi ambao unaendelea.
“Uchunguzi umebaini kuwa uvamizi huo haukutekelezwa na washukiwa hao watatu peke yao. Maafisa wa upelelezi wanaendeleza uchunguzi kuwatambua na kuwatia nguvuni wahusika wote kwenye uvamizi huo,” ilisema DCI kupitia kwa taarifa.
Watatu hao sasa wanajiunga na wengine wawili waliokamatwa awali, huku idra ya DCI ikiwahakikishia wananchi kuwa wale wote waliohusika watachukuliwa hatua.
“Sehemu za ibada, ni za amani na kutafakari na yeyote ambaye atavuruga usalama wa umma au mikusanyiko ya umma, atachukuliwa hatua za kisheria,” iliongeza DCI.