Ruto: Serikali italinda haki ya kikatiba ya kila Mkenya

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto apokea ripoti ya KNCHR katika Ikulu ya Nairobi.

Rais William Ruto, amesema serikali imejitolea kulinda kikamilifu haki ya kila mkenya ya kushiriki maandamano kwa njia ya amani.

Akizungumza Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi kwenye hafla ya kupokea ripoti kuhusu mikakati ya kuwafidia wahanga wa dhuluma za haki za kibinadamu iliyowasilishwa na Tume ya kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR), kiongozi wa taifa alidokeza kuwa, wakenya wamepoteza maisha, mali kuharibiwa na wengine kujeruhiwa kwenye maandamano ya amani ambayo baadaye hugeuka kuwa ghasia.

“Nyakati zingine maafisa wa usalama wametumia nguvu kupita kiasi wanapokabiliana na maanadamano, hatua inayosababisha ukiukaji wa haki za binadamu na maafa,” alisema Rais Ruto.

Hata hivyo, kiongozi wa taifa alisema serikali imeazimia kuchukua hatua, na itatekeleza kikamilifu ripoti hiyo ya KNCHR.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa KNCHR Claris Ogangah, alisema ripoti hiyo inachangia pakubwa kwa mchakato wa uponyaji wa kitaifa uliojikita katika ukweli, kutambua na kumbukumbu.

Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na kiongozi wa chama cha ODM Oburu Oginga miongoni mwa wengine.

Share This Article