NTSA yafuta leseni ya kuhudumu ya Nicco Movers 1

Tom Mathinji
1 Min Read

Halmashauri ya Uchukuzi na usalama Barabarani (NTSA), imefutilia mbali leseni ya kuhudumu ya Chama cha Ushirika cha Nicco Movers 1, kufuatia kifo tatanisgi cha mwanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu KMTC.

Kupitia kwa taarifa siku ya Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa NTSA, aliagiza magari yote yanayohudumu chini ya leseni ya chama hicho kusitisha huduma zao mara moja baada ya kukagua magri hayo.

“Kama sehemu ya uchunguzi kuhusu tukio hilo la kushangaza lililosababisha kifo cha Eugene Mutuku, mwanafunzi wa KMTC, NTSA ilifanya uchunguzi wa operesheni wa magari hayo,” ilisema NTSA kwenye taarifa.

Kulingana na NTSA, uchunguzi wao uligundua kuwa maafisa wasimamizi wa chama hicho cha ushirika, wamepoteza udhibiti wa magari hayo, hawazingatii sheria za usalama na hawajaonyesha nia yoyote ya kushughulikia swala hilo.

Vile vile NTSA ilidokeza kuwa magari yanayohudumu chini ya chama hicho sio salama na ni hatari watumiaji wa barabara.

“Ni kutokana na sababu hizi, NTSA imeazimia kufutilia mbali leseni ya kuhudumu ya chama cha Nicco Movers 1, mara moja,” ilisema NTSA.

Halmashauri hiyo imewaagiza maafisa wa utekelezaji sheria kukamata magari ya chama hicho ambayo yatakiuka agizo hilo.

TAGGED:
Share This Article