Huzuni na majonzi vilitanda wakati wa ibada ya vifo vya wanafunzi 16 waliofariki katika mkasa wa moto uliotokea katika shule ya Utumishi Girls Academy, mjini Gilgil katika kaunti ya Nakuru Mei 28 mwaka huu.
Ibada hiyo iliandaliwa katika uwanja wa Gilgil leo Ijumaa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkewe Rais Rachel Ruto, Waziri wa Elimu Julius Ogamba, Gavana wa Nakuru Susan Kihika, Seneta Tabitha Karanja na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna miongoni mwa wengine.
Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri Ogamba, Rais William Ruto aliahidi kwamba serikali yake inafanya kila iwezalo kukomesha mikasa ya moto ya aina hiyo shuleni.
Alizifariji familia zilizoathirika akizitakia uponyaji wa haraka.
Ujumbe sawia ulitolewa na Bi. Rachel aliyezitaka familia zilizowapoteza wapendwa wao kumtumainia Mwenyezi Mungu kwani ni yeye pekee atakayewafariji.
“Mwenyezi Mungu yu karibu na waliokufa moyo; huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa. Mateso ya mwadilifu ni mengi, lakini Mwenyezi Mungu humwokoa kutoka yote,” Bi. Rachel aliziomboleza familia hizo wakati akinukuu kitabu cha Zaburi 34:18.
Kwa upande wake, Waziri Ogamba alilaani mkasa huo ambao alisema ulisababishwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo na kuwataka wanafunzi kutafuta njia mbadala za kuelezea malalamishi yao.
Alionya kuwa wanafunzi watakaopatikana wakijihusisha katika vurugu na vitendo vya utovu wa nidhamu akisema watachukuliwa hatua kali.
Aidha, aliwataka wadau wote wakiwemo walimu, wazazi, maafisa wa serikali na wadau wengine kuangazia namna wanavyoshughulikia makuzi ya watoto nchini.
Alidokeza kuwa serikali ina mipango ya kuunda jopo litakalobaini chanzo cha vurugu shuleni na namna ya kukabiliana nazo.
Kwa upande wake, Seneta Sifuna alitoa wito kwa serikali kufanya kila iwezalo kukomesha mikasa ya aina hiyo kutokea nchini.
“Hadi lini? Na huu uwe mkasa wa mwisho kushuhudiwa nchini,” alisema Seneta Sifuna katika wito uliorindima kwenye ibada hiyo.
Kwenye hotuba yake, Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Kiambu Anne Wamuratha alionya dhidi ya kulaumiana na kuto wito kwa wadau wote kushikana mikono kutafuta njia za kukomesha changamoto zinazozikumba shule.
Wakati wa mkasa wa moto uliotokea katika shule ya Utumishi Girls Aacademy Mei 28, wanafunzi 79 pia walijeruhiwa.
Wanafunzi 9 wanaoshukiwa kuwasha moto na kutekeza bweni la shule hiyo wanazuiliwa ili kupisha uchunguzi wa kina.
Tangu tukio hilo, shule 204 zimefungwa nchini kutokana na visa vya utovu wa nidhamu na vurugu za wanafunzi huku shule 59 kati ya shule hizo zikirejelea masomo.