Umoja wa Ulaya (EU) utawekeza shilingi bilioni 15.3 chini ya mpango wa kidijitali wa EU na Kenya ili kuchochea ukuaji wa kidijitali, hatua itakayopanua uunganishaji wa mtandao, ukuaji wa biashara na utoaji nafasi za ajira kwa vijana.
Akizungumza nchini Ubelgiji siku ya Jumatatu, Rais William Ruto alisema kupitia uwekezaji huo, EU itaweka nyaya za majini za dijitali ambazo zitaunganisha mataifa ya Djibouti, Somalia, Kenya na Tanzania, na kuimarisha uunganishaji wa mtandao na kuifanya Kenya kuwa kitovu cha dijitali katika kanda hii.
Kiongozi huyo wa taifa aliyasema hayo aliposhiriki mazungumzo na Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya Henna Virkkunen, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na EU katika sekta za biashara, uvumbuzi na uchumi wa dijitali.
“Tumefanyia marekebisho utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Kenya na EU, ambapo mauzo ya Kenya katika EU yameongezeka kwa asilimia 20 tangu kubuniwa kwake,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa Kenya na EU unaendelea kuzaa matunda hasa katika kupanua uwekezaji, kuimarisha uvumbuzi na ustawi wa pamoja.
Siku ya Jumapili, Rais Ruto alizanza ziara ya kiserikali katika EU, akitarajiwa kuzuru nchi za Ubelgiji, Finland na Norway.