Serikali imesema itajizatiti kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilishwa kwa wakati ndani ya kipindi cha matumizi ya pesa za serikali.
Akizungumza mjini Awendo, kaunti ya Migori wakati wa uzinduzi wa barabara ya Kanyawanga–Dede–Rapogi ya umbali wa kilomita 32, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema serikali inaazimia kukamilisha miradi jinsi ilivyopangwa.
Amesema kuwa ustawi wa miundombinu umeendelea kutekeleza jukumu muhimu katika kuimarisha uunganishaji, kufanikisha biashara na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kote nchini.
“Ukamilishaji wa mradi huu unaziba pengo la kutengwa na kuimarisha sekta ya uchukuzi katika kanda hii,” alisema Mbadi.
Kulingana naye, mipango ya maendeleo ya kitaifa inatekelezwa kote nchini, yakiwemo maeneo ambayo yamekuwa yakikosa uwekezaji wa kutosha ili kuimarisha maendeleo yenye usawa na kuhakikisha kwamba fursa za kiuchumi zinasambazwa kwa usawa.
Aliandamana na Gavana wa Migori Ochillo Ayacko, Seneta Moses Kajwang’, Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo na wawakilishi wadi miongoni mwa wengine.