Rais William Ruto amewatuza wanamichezo waliofanya vyema kimataifa kitita cha shilingi milioni 32 siku ya Ijumaa wakati wa hafla ya kuzindua jengo la Talanta Plaza eneo la Upper hill kaunti ya Nairobi.
Wanariadha walioshiriki makala ya 19 ya mashindano ya Riadha Duniani mjini Budapest,Hungary ndio waliopokea donge nono,kila mshindi wa nishani ya dhahabu alitunukiwa shilingi milioni 2 ,washindi wa nishani za fedha wakapokea shilingi milioni 1 nukta 5 kila mmoja huku washindi wa medali za shaba wakipokea shilingi milioni 1 kila mmoja.
Wanariadha wote waliofuzu kwa fainali katika mashindano ya Budapest watapokea shilingi elfu 50.
Wanariadha walioshiriki michezo ya jumuiya ya madola kwa chipukizi nchini Trinidad na Tobago pia walituzwa kitita cha shilingi milioni 3, huku washindi wa dhahabu wakipokea laki tatu unusu.
Mabingwa wa bara Afrika katika Voliboli ya akina dada,Malkia Strikers walituzwa shilingi milioni 4 nukta 45 kwa jumla,wachezaji wakipokea shilingi lmilioni 2 nukta 8 na milioni 1 nukta 1 kwa maafisa wa kiufundi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Rais Ruto aliahidi kuwa serikali yake itaendelea kutilia mkazo na kutoakipa umbele kwa sekta ya michezo nchini na kutambua vipaji.
Jumba la Talanta lililo na orofa 16 lilianza kujengwa mwaka 2014 na kamatiu ya Olimpiki nchini NOCK, ujenzi wake ulikwama kwa muda kutokana na ukosefu wa pesa kabla ya serikali kuingilia kati mwaka 2019 walipolinusuru dhidi ya kuuzwa kwa kushindwa kuwalipa wakandarasi.
Jengo hilo ambalo litakuwa makao makuu mapya ya wizara ya michezo ,masuala ya vijana na sanaa na mashirikisho ya michezo limegharimu kima cha shilingibilioni 1 nukta 2.