Kampuni ya China ya Changan Automobile iliyoko katika manispaa ya Chongqing imetangaza takwimu zake za mauzo za Aprili zikionyesha ukuaji huku magari ya nishati mpya na masoko ya kimataifa yakichochea kasi ya kampuni hiyo.
Mwezi Aprili, Changan iliuza magari 209,500, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Mauzo ya magari ya nishati mpya yalifikia magari 94,200, yakiongezeka kwa asilimia 32.2, huku mauzo ya nje yakipanda kwa asilimia 69.9 hadi magari 72,700.
Chapa tatu za magari ya nishati mpya za Changan zote zilionyesha mafanikio makubwa. Deepal iliuza magari 33,187, ongezeko la asilimia 64.8, huku modeli ya Deepal S05 ikiendelea kuuza zaidi ya magari 10,000 kwa mwezi na kufanya jumla ya mauzo ya chapa hiyo kuvuka magari 200,000.
Avatr iliuza magari 5,279, ikichochewa na uzinduzi wa modeli mpya pamoja na uzinduzi wa kwanza barani Asia wa gari la dhana la VISION XPECTRA katika maonesho ya Auto China 2026, hatua iliyosaidia kuimarisha nafasi yake katika soko la magari ya hadhi ya juu. Mauzo ya Qiyuan yalifikia magari 32,118.
Katika kuongeza kasi ya ukuaji wa chapa zake za magari ya nishati mpya, Changan ilitangaza kuunganisha kwa pamoja shughuli za Deepal na Avatr. Ingawa kila chapa itaendelea kuwa na nafasi yake sokoni, mahusiano ya wateja na shughuli za mauzo zitaendelea kujitegemea, kampuni hizo zitashirikiana katika utafiti na maendeleo, mnyororo wa usambazaji pamoja na uzalishaji.
Changan inalenga kujenga kundi la chapa za magari za hadhi ya kati hadi ya juu lenye mauzo ya zaidi ya magari milioni 1.5 kwa mwaka, huku masoko ya nje yakichangia zaidi ya asilimia 40 ya mauzo yote.
Malengo hayo yanaendeshwa kwa kiasi kikubwa na upanuzi wa haraka wa masoko ya kimataifa. Tangu kuzindua mkakati wake wa kimataifa mwaka 2023, mauzo ya nje ya Changan yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, yakifikia magari 358,000 mwaka 2023, magari 536,000 mwaka 2024 na magari 637,000 mwaka 2025, sawa na jumla ya magari milioni 1.531 ndani ya miaka mitatu.
Katika maonesho ya Auto China 2026, kampuni hiyo iliongeza zaidi matarajio yake ya kimataifa kwa kutangaza mpango wa kuongeza mara mbili mauzo ya nje hadi magari milioni 1.5 ifikapo mwaka 2030, huku ikijiwekea lengo la juu zaidi la magari milioni 1.8.
Kupungua kwa mahitaji ya magari ya abiria ndani ya China kunazisukuma kampuni za magari za China, ikiwemo Changan, kupanua shughuli zao nje ya nchi.
Cui Dongshu, katibu mkuu wa chama cha magari ya abiria cha China, alisema kuwa mauzo ya rejareja nchini China yalishuka kwa asilimia 18 hadi magari milioni 5.628 kati ya Januari na Aprili 2026, huku mauzo ya nje yakiongezeka kwa asilimia 52 hadi magari milioni 3.28, kiwango ambacho ni cha juu katika miaka ya hivi karibuni.
Mauzo yanaendelea kuwa kipimo muhimu cha utendaji wa kampuni za magari hasa wakati ushindani wa sekta hiyo duniani ukiendelea kuongezeka. Akizungumza katika uzinduzi wa mkakati wa kimataifa wa Changan mwezi Aprili, Mwenyekiti wa kampuni hiyo Zhu Huarong alisema sekta ya magari inaingia katika kipindi cha “wanaobaki ni wenye nguvu zaidi” ambacho kitaendelea ndani ya miaka mitatu hadi mitano ijayo.
Alisema kuwa mauzo ya magari milioni 8 hadi 10 kwa mwaka yanaashiria uongozi wa sekta hiyo, milioni 5 hadi 7 yanaonyesha uwezo wa kuendelea kuishi kwa uthabiti, huku milioni 3 hadi 3.5 zikionyesha kiwango cha chini cha kuendelea kuhimili ushindani. Alisisitiza umuhimu wa kampuni hiyo kuweka malengo makubwa zaidi ya ukuaji.
Changan inalenga kuuza magari milioni 4 duniani ifikapo mwaka 2030, pamoja na lengo la juu zaidi la zaidi ya magari milioni 5.
Kwa kuzingatia mauzo ya jumla ya Changan ya magari milioni 2.913 mwaka 2025, kufikia mauzo ya magari milioni 4 ndani ya miaka mitano kutahitaji wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 6 kila mwaka, huku kufikia magari milioni 5 kutahitaji ukuaji wa zaidi ya asilimia 11 kwa mwaka.
Kwa hisani ya iChongqing.info