Mahakama Kuu yasitisha karantini ya wagonjwa wa Ebola Kenya

Mahakama pia imesimamisha usafirishaji wa wagonjwa wa Ebola hadi nchini Kenya chini ya mpango huo, unaosemekana kuafikiwa baina ya Kenya na Marekani.

Dismas Otuke
1 Min Read

Mahakama Kuu ya Kenya imesitisha kwa muda pendekezo la serikali ya Marekani la kufungua kituo cha karantini nchini Kenya, kitakachotumiwa kuwatenga raia wake watakaobainika kuambukizwa ugonjwa wa Ebola.

Mahakama pia imesimamisha usafirishaji wa wagonjwa wa Ebola hadi nchini Kenya, chini ya mpango huo ambao uliripotiwa kuafikiwa baina ya Kenya na Marekani.

Mamlaka nchini Kenya hazijazungumzia suala hilo waziwazi.

Kesi ya kupinga karantini hiyo iliwasilishwa kortini na shirika la Katiba Institute, ambalo linasema kuwa serikali haikushirikisha umma inavyohitajika kabla ya kuafikia uamuzi huo.

Aidha, Katiba Institute wanahoji usiri uliopo kwenye mpango huo kati  ya Kenya na Marekani.

Kulingana na shirika hilo, hatua hiyo huenda ikawa tishio kubwa kwa Wakenya kutokana na msambao wa haraka wa Ebola.

Chama cha Madaktari nchini Kenya, KMPDU pia kimepinga vikali mpango huo kikiutaja kuwa hatari kwa afya ya umma.

“Kama walinzi wakuu wa mfumo wa afya nchini Kenya, tunasikitishwa mno na utayari unaoonekana wa serikali kuhatarisha usalama wa kibiolojia wa taifa na maisha ya raia wake kwa ajili ya misaada ya kigeni,” alilalama Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah kwenye taarifa.

 

Share This Article