Uteuzi wa kitaifa kwa wanariadha chipukizi kuanza leo Nyayo

Chama cha Riadha Kenya kinatarajiwa kuwateua wanariadha wapatao 30 kwa mashindano ya Dunia, yatakayoandaliwa Mjini Eugene nchini Marekani baina ya Agosti 5 na 9 mwaka huu.

Dismas Otuke
2 Min Read

Majaribio ya kitaifa ya siku tatu kuteua kikosi cha wanariadha wasiozidi umri wa miaka 2 kwa mashindano ya dunia yataanza leo Alhamisi, Mei 21 hadi Jumamosi hii uwanjani Nyayo.

Bingwa mtetezi wa Dunia katika mbio za mita 5000 Andrew Kiptoo Alamisi, na bingwa wa Afrika wa mita 3000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 Cynthia Chepkirui ni miongoni mwa wanariadha watakaoshiriki.

Kiptoo aliyeshinda dhahabu ya Dunia mwaka 2024 mjini Lima, Peru atawania tiketi ya kutetea taji lake la mita 5,000 pamoja na wanariadha wengine 18, wanaowania nafasi mbili za kufuzu.

Chepkirui aliye na umri wa miaka 17 na aliyeshinda dhahabu ya Afrika mwaka jana nchini Nigeria, atakabiliana na mshindi wa nishani ya shaba ya Afrika katika mita 3000 kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20 Joyline Chepkemoi na Sheila Chepng’eno, miongoni mwa wengine.

Bingwa wa Afrika kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 18 katika mita 2000 kuruka viunzi na maji Emmanuel Lemiso, atatimka mita 3000 kuruka viunzi na maji pamoja na Felix Kiptoo na Evans Kipkemboi miongoni mwa wengine.

Chama cha Riadha Kenya kinatarajiwa kuwateua wanariadha wapatao 30 kwa mashindano ya Dunia yatakayoandaliwa Mjini Eugene nchini Marekani baina ya Agosti 5 na 9 mwaka huu.

Share This Article