Timu ya taifa ya Kenya kwa wasichana chini ya umri wa miaka 17, imeendeleza mazoezi yake Jumatano jijini Kampala nchini Uganda ili kujiandaa kwa mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji mwishoni mwa juma hili.
Junior Starlets wanaofunzwa na Mildred Checha waliwasili Uganda juzi Jumanne.
Kenya itachuana na Uganda Mei 22 jijini Kampala, kabla ya duru ya pili kupigwa Nairobi, wiki moja baadaye.
Uganda iliwatema Zimbabwe katika raundi ya kwanza mabao 6-1 wakati Kenya ikiwabwaga Namibia kwa jumla ya magoli 7-1.
Mshindi wa mechi hiyo atakuwa na miadi na aidha Tanzania au Afrika Kusini katika raundi ya tatu na ya mwisho.
Fainali za Kombe la Dunia zitaandaliwa nchini Morocco kati ya Oktoba 17 na Novemba 7 mwaka huu.