Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 utakuwa huru, wa amani na haki.
Matamshi yake yanakuja siku chache baada ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta kuonya dhidi ya matumizi ya semi za chuki na kikabila, akionya kuwa zinaweza kuitumbukiza nchi hii katika vurugu sawia na za mwaka 2007.
“Tunaenda kuwa na uchaguzi, na utakuwa wa amani, hakutakuwa na vurugu, na utakuwa huru na wa haki,” aliahidi kiongozi wa nchi wakati wa hafla ya kuliombea taifa iliyofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi leo Alhamisi.
“Hii ni kwa sababu kile ambacho Mungu ameamua, hakuna binadamu anaweza kukibadilisha…Ile Mungu ameamua ndio itafanyika. Kama Mungu ameamua Ruto atapata muhula wa pili, hicho ndicho kitakachofanyika. Kama Mungu ameamua vingine, hicho ndicho kitakachofanyika, na tutasonga mbele kama nchi.”
Hakikisho la Ruto huenda likautuliza upande wa upinzani ulioelezea wasisi kutokana na matamshi ya baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza kwamba kutakuwa na wizi wa kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Wa hivi punde kutoka madai ya wizi wa kura alikuwa Naibu Gavana wa kaunti ya Kakamega Ayub Savula.
Ni madai ambayo yamekemewa vikali na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambayo imeahidi kufanya kila iwezalo kuhakikisha uchaguzi ujao ni huru na wa haki.