Punde taarifa za mkasa wa moto zilipotokea, wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru walijawa na hofu.
Mzazi mmoja alinukuliwa akisema alipokea taarifa hizo majira ya saa kumi alfajiri, na mara moja, alifunga safari ya kuelekea Gilgil kubaini hali ya mwanawe.
Kwa bahati nzuri, mwanawe alinusurika ila alipata majeraha ya hapa na pale.
Kwake, hiyo ilikuwa bora kwani wasemavyo, heri nusu shari kuliko shari kamili.
Nje ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2020, wazazi walifika kwa wingi wao, wakitokea kila pembe ya nchi, nyuso zao zikiwa zimesheheni huzuni na mashaka mengi.
Mashaka ya kutojua ikiwa watapata fursa ya kuwaona tena wanao ambao walikuwa wenye afya nzuri na tabasamu mara ya mwisho walipoonana.
“Nifahamisheni ikiwa mwanangu yu hai au ameaga dunia,” mzazi mmoja alinukuliwa akiwaomba maafisa wa usalama walioshika doria.
Kwa bahati mbaya, majira ya saa tano asubuhi leo Alhamisi, mashaka ya baadhi ya wazazi yaligeuzwa kuwa majonzi baada ya Waziri wa Elimu Julius Ogamba kuthibitisha kuwa wanafunzi 16 walifariki kutokana na mkasa huo.
Wengine 79 walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Kufikia wakati akiwahutubia wanahabari, Ogamba alisema ni wanafunzi 7 pekee ambao walikuwa bado wamelazwa hospitalini.
71 walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku mwanafunzi mmoja akichukuliwa na mzazi wake.
Shule ya Utumishi Girls Academy ina jumla ya wanafunzi 815, ila ni wanafunzi 808 waliokuwa shuleni wakati wa mkasa.
7 walikuwa wameenda nyumbani kwa sababu mbalimbali.
Punde baada ya taarifa za kufariki kwa wanafunzi 16 kuchipuza, baadhi ya wazazi walielemewa na uchungu mwingi huku wakipkiga ukelele uliotikisa anga ya eneo zima la Gilgil.
Ni ukelele uliodhihirisha uchungu wa kumpoteza mwana uliyefumkana naye akiwa mzima, lakini wakati ujao ukikutana naye, uhai wake umegeuka kuwa mauti.
Mamlaka zinasema uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo unaendelea.