Ruto aipongeza Arsenal kwa kushinda Ligi Kuu Uingereza

Vijana wake Mikel Arteta walitangazwa mabingwa wa Ligi Kuuu ya Uingereza msimu wa mwaka 2025/2026 baada ya Man City kutoka sare ya bao moja ugenini dhidi ya Bournemouth jana Jumanne.  

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameilimbikizia sifa sufufu timu ya Arsenal kwa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya ngoja ngoja ya miaka 22.

Vijana wake Mikel Arteta walitangazwa mabingwa wa Ligi Kuuu ya Uingereza msimu wa mwaka 2025/2026 baada ya wapinzani wao wa karibu Man City kutoka sare ya bao moja ugenini dhidi ya Bournemouth jana Jumanne.

Hilo ni taji la kwanza ambalo Arsenal imeshinda tangu msimu wa mwaka 2003/2004.

Ni ngoja ngoja ya muda mrefu ambayo Rais Ruto alionekana kukiri kwenye ujumbe wake wa pongezi.

“Imekuwa safari ndefu kuishabikia Klabu ya Soka ya Arsenal, kutoka nyakati za mahangaiko na kuchabangwa, na misimu ya kumakinika iliyofuata na kutamba tena hadi kushinda Ligi Kuu ya Uingereza,” alisema Ruto ambaye ni shabiki sugu wa The Gunners.

“Wakati wa kipindi hicho, tumeshuhudia nguvu ya matumaini, uthabiti, shabaha na bidii ya mchwa ikifanyiwa kazi, na kutazama timu yenye utaalam wa kujituma ikipambana dhidi ya miamba wa kuotea mbali, mechi baada ya mechi. Usiku huu, timu imeshinda tuzo kuu. Timu imeibuka mshindi. Imani na dhamira yake vimedhihirika,” aliongeza Rais Ruto wakati akiipongeza Arsenal.

Kwenye mechi ya hiyo jana dhidi ya Bournemouth, Man City walikuwa na shinikizo kubwa kwani walifahamu fika kuwa ni ushindi pekee ambao ungewaweka kwenye kinyang’anyiro na kulazimu mabingwa kubainika Jumapili, Mei 24, wakati wa mechi za kufunga msimu.

Hata hivyo, City walijipata nyuma baada ya Eli Junior Kroupi kupachika bao la ufunguzi kwa wenyejeji.

Vijana wa Pep Guardiola walijituma na hatimaye kusawazisha kupitia kwa Erling Halaand kunako dakika ya sita ya muda wa mazidadi.

Arsenal wameshinda taji la Ligi Kuu ya Uingereza mara nne sasa ikiwa ni pamoja na mwaka 1997/1998, 2001/2002 na 2003/2004.

The Gunners wanaongoza jedwali kwa alama 82 baada ya mechi 37, wakifuatwa na Man City wenye alama 78, alama 10 juu ya Man United iliyo ya tatu.

 

Share This Article