Wafanyabiashara wakadiria hasara mgomo wa matatu ukiingia siku ya pili

Martin Mwanje
2 Min Read

Biashara nyingi ziliendelea kuhisi athari ya mgomo wa matatu unaoendelea nchini kulalamikia ongezeko la bei ya mafuta. 

Jijini Nairobi sawia na maeneo mengine, wahudumu wa biashara zikiwemo supamaketi, walikadiria hasara ya mamilioni ya pesa kufuatia kufungwa kwa biashara zao kwa hofu ya wahuni kupora mali yao.

Licha ya tahadhari hiyo, kulikuwa na ripoti za supamaketi na maeneo mengine kadhaa ya biashara kuporwa wakati wa maandamano ya hapo jana.

Huku mgomo wa matatu ukiingia siku ya pili, wafanyabiashara wengi waliendelea kuchukua tahadhari na kuendelea kufunga biashara zao hadi hali ya kawaida itakaporejea.

Katika miji ya Ruiru na Thika, biashara ziliendelea kufungwa huku wahudumu wa matatu na baadhi ya wakazi wakikosa kukanyaga guu katika miji hiyo.

Miji hiyo, ambayo kwa kawaida huwa na pirikapirika nyingi, ilisalia mahame huku maduka mengi yakifungwa kwa hofu ya uporaji.

Barabara kadhaa nazo zilifungwa na vijana waliovuruga usafiri.

Awamu nyingine ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika leo Jumanne kati ya serikali na wadau wa sekta ya uchukuzi wa umma kuhusiana na ongezeko la bei ya mafuta.

Wahudumu wa uchukuzi wa umma wanasema bei za juu za mafuta zimegeuka kuwa mwiba katika uendeshaji wa biashara zao.

Kwa upande wake, serikali imehusisha bei hizo na mgogoro wa Mashariki ya Kati unaozihusisha nchi za Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Juhudi za serikali kutafuta suluhu ya mgomo wa matatu ziliambulia patupu baada ya mazungumzo ya hiyo jana kugonga mwamba.

 

Share This Article