Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki pamoja na kundi la mawaziri wameagizwa kuanzisha mazungumzo na wahudumu wa sekta ya umma, watengenezaji bidhaa na wadau wengine kuhusu bei za mafuta.
Agizo hilo limetolewa na Rais William Ruto wakati ambapo serikali inaendelea kushughulikia bei za mafuta ambazo inasema zimeongezeka kutokana na mzozo unaoshuhudiwa Mashariki ya Kati.
Ruto kwa sasa yuko kwenye ziara ya kiserikali nchini Azerbaijan.
Akizungumza katika kaunti ya Tharaka Nithi, Prof. Kindiki alisema Rais amemuagiza yeye pamoja na mawaziri John Mbadi (Fedha), Davis Chirchir (Barabara na Uchukuzi), Opiyo Wandayi (Nishati) na Kipchumba Murkomen (Usalama wa Taifa) kushiriki meza ya mazungumzo na wadau katika sekta ya petroli na uchukuzi kutafuta suluhu ili kudhiti bei za mafuta.
Alidokeza kuwa serikali inafahamu mzigo mkubwa ambao umelimbikiziwa Wakenya kutokana na bei za juu za mafuta, lakini akasisitiza kuwa hali hiyo imesababishwa na mgogoro unaoshuhudiwa Mashariki ya Kati ambao pia umeathiri mataifa mengine duniani.
Alipongeza serikali ya Rais Ruto aliyosema ilipunguza bei za mafuta kutoka shilingi 218 kwa lita hadi shilingi 171 kwa lita.
Wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma nchini Kenya, waliandaa mgomo siku ya Jumatatu wakilalamikia bei ya juu ya mafuta huku wakisambaratisha shughuli za uchukuzi kote nchini.