Raia wa Rwanda Felicien Kabuga ambaye amekuwa akijaribiwa katika mahakama ya ICC kuhusiana na mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda amefariki.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, Kabuga alifariki akiwa na umri wa miaka 93, akiendelea kupokea matibabu jijini Hague nchini Uholanzi.
Félicien Kabuga alishtakiwa kwa makosa ya mauaji ya halaiki, uchochezi wa kufanya mauaji hayo, njama ya kutekeleza mauaji ya halaiki, pamoja na mateso, maangamizi na mauaji.
Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa ya Kesi za Jinai ilisema imeamuru uchunguzi kuhusu mazingira ya kifo chake.
Kabuga alikuwa mmoja wa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa zaidi duniani, akilaumiwa kwa kuhamasisha na kufadhili mauaji yaliyotokea kati ya Aprili na Juni mwaka 1994 nchini Rwanda.
Wahutu wenye msimamo mkali waliwaua Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani wapatao 800,000 ndani ya siku 100.
Mauaji hayo ya halaiki yalichochewa na kisa cha ndege iliyombeba Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana kupigwa risasi angani juu ya mji mkuu Kigali tarehe 6 Aprili 1994 ambapo kiongozi huyo Mhutu aliuawa.
Kabuga alikuwa mshirika wa karibu wa Habyarimana na chama chake cha kisiasa.
Kabuga alikwepa kukamatwa kwa zaidi ya miongo miwili baada ya mauaji hayo ya halaiki, akitumia pasipoti bandia mbalimbali na kusaidiwa na mtandao wa washirika wake wa zamani kutoka Rwanda.
Hati ya kukamatwa kwake ilitolewa mwaka 2013, huku zawadi ya dola milioni tano za Marekani ikitangazwa kwa yeyote angeyetoa taarifa za kukamatwa kwake.
Hatimaye alikamatwa mwaka 2020 nchini Ufaransa na kuhamishiwa The Hague, Uholanzi. Kesi yake ilianza mwaka 2022 ambapo alikana mashtaka yote dhidi yake.
Hata hivyo, baadaye iliamuliwa kuwa hakuwa na uwezo wa kusimama kizimbani kutokana na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu wa dementia, uamuzi uliowakasirisha manusura wengi wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda, ambao walihisi kuwa makosa yake yalistahili adhabu ya juu zaidi.
Kabuga pia alionekana kuwa mgonjwa sana kiasi cha kutoweza kurejeshwa Rwanda na kutokana na kukosekana kwa nchi iliyokuwa tayari kumpokea, Kabuga aliendelea kubaki katika kituo cha Umoja wa Mataifa mjini The Hague.