Chama cha kibiashara na Wenye Viwanda nchini Kenya (KNCCI), kimewatahadharisha wakenya kuwa bei za bidhaa huenda zikaongezeka kwa asilima 7, kutokana na ongezeko la bei za bidhaa za mafuta.
Kulingana na chama hicho, gharama ya uchukuzi itapanda kwa kati ya asilimia 10 na 20, huku gharama ya utengenezaji bidhaa na usambazaji wa bidhaa za kilimo ikipanda kwa asilimia 12.
Rais wa chama hicho Dkt. Erick Ruto, alidokeza kuwa nyongeza ya mafuta ya diesel ambayo ndio uti wa mgongo katika sekta za uchukuzi, kilimo, utengenezaji bidhaa, ujenzi na biashara, itasababisha kupanda haraka kwa gharama ya uchukuzi na uzalishaji wa bidhaa muhimu nchini Kenya.
Siku ya Alhamisi, Halmashauri ya Nishati na kudhibiti mafuta (EPRA), ilipandisha bei ya bidhaa za mafuta, ambapo lita moja ya mafuta ya Super Petrol iliongezeka kwa shilingi 16 na diesel ikipanda kwa shilingi 46.26.
Kutokana na nyongeza hiyo, chama cha wamiliki wa magari ya uchukuzi wa umma, kimesema kitaongeza nauli kwa asilimia 50 kuanzia Jumatatu Mei, 18, 2026.
Jijini Nairobi lita moja ya petroli inauzwa kwa shilingi 214 na senti 25 huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 242 na centi 92 kwa lita.