Vikosi vya kijeshi vya Nigeria na Marekani vimemuua kamanda mmoja mkuu wa ISIS, kwenye operesheni ya pamoja iliyotekelezwa Ijumaa.
Huku akitangaza habari za kuuawa kwa Abu-Bilal al-Minuki, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kamanda huyo wa pili wa ISIS, alikuwa mtu hatari sana aliyewadhuru raia wa Afrika na kuwashambulia Wamarekani.
“Abu Bilal al-Minouki hataweza tena kuwadhuru watu wa Afrika wala kupanga mashambulizi dhidi ya Wamarekani,” alisema Rais Trump kupitia ukurasa wake wa Truth.
Hata hivyo, Trump hakutaja eneo la shambulizi hilo, akisema Minouki alidhani atajificha Afrika lakini hakujua Marekani ilikuwa na habari kumhusu.
Taarifa hizo za Trump pia zimethibitishwa na Rais wa Nigeria Bola Tinubu, akisema kuwa Jeshi la Nigeria, likishirikiana kwa karibu na Jeshi la Marekani, liliendesha operesheni ya pamoja ambayo ilikuwa pigo kubwa katika uongozi wa kundi hilo.
Al-Minuki, ambaye ni raia wa Nigeria, alitajwa kuwa gaidi wa kimataifa na utawala wa Rais Mstaafu wa Marekani Joe Biden mwaka 2023.