Watu 65 wafariki kutokana na Ebola DRC

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu 65 wafariki kutokana na Ebola nchini DRC.

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (CDC), kimethibitisha kuwa watu 65 wamefariki kutokana na mlipuko mpya wa Ebola katika mkoa wa Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Aidha, kulingana na tarifa hiyo ya Afrika CDC, watu wengine 246 wameambukizwa ugonjwa huo, hususan katika maeneo ya uchimbaji dhahabu ya Mongwalu na Rwampara.

Kituo hicho kilisema kitaandaa mkutano na serikali ya DRC, majirani Rwanda na Sudan Kusini pamoja na washirika wengine wa kimataifa, kujadili juhudi za kukabiliana na mlipuko huo  na uchunguzi wa mpakani.

Ugonjwa wa Ebola uligunduliwa mara ya kwanza mwaka wa 1976 nchini DRC na inaaminika kuwa ilisambazwa kutoka kwa popo. Huu ni mlipuko wa 17 wa ugonjwa huo hatari nchini humo.

Dalili za mapema za ugonjwa huu ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, uchovu, maumivu ya kichwa na koo.

Hadi kufikia sasa hakuna tiba iliyothibitishwa ya Ebola.

TAGGED:
Share This Article