Ykee Benda aelezea sababu za kutaka kushirikiana na Chameleone

Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano kuhusu wasanii wa muda mrefu anaotaka kushirikiana nao.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Ykee Benda ameelezea sababu za kutaka kushirikiana na mwanamuziki nguli Jose Chameleone.

Akizungumza kwenye mahojiano kuhusu wasanii wa muda mrefu anaotaka kushirikiana nao, Ykee Benda alitaja wasanii kama Juliana Kanyomozi, Cindy Sanyu na Eddy Kenzo, akisisitiza sana kuhusu Chameleone.

Wasanii wengi huingia kwenye ushirikiano kwa nia ya kuongoza orodha za mashindano ya nyimbo, mitindo na ushawishi wa ulimwengu mzima lakini kwa Ykee Benda, ushirikiano na Jose Chameleone una umuhimu zaidi.

Alisema sababu zake za kutaka kufanya kazi na Chameleone ni tofauti na sababu zake za kushirikiana na wengine akiongeza kwamba, “Wakati babangu Mowzey Radio alifariki kabla ya kushirikiana naye, msanii anayekaribia kiwango hicho ni Jose Chameleone.”

Ykee alikuwa anamtizamia sana marehemu Mowzey Radio ambaye wengi walikuwa wanamtambua kama mmoja wa waandishi wa nyimbo bora zaidi nchini Uganda, kando na kuwa mwimbaji mzuri.

Radio anazungumziwa hadi sasa nchini Uganda kutokana na weledi wake na kwa Ykee, hisia kali zinatokana na kukosa fursa ya kushirikiana na Radio kabla ya kifo chake.

Huku akifafanua kwamba halinganishi wasanii, Ykee alisema kwamba kwa maoni yake, Chameleone anawakilisha daraja la karibu kabisa kwa kile alichokosa.

Mowzey Radio au Moses Ssekibogo, alikuwa akiimba na Weasel Manizo katika kundi walilolirejelea kama “Radio & Weasel” lakini alifariki Februari Mosi mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 33.

Alihusika kwenye ugomvi kwenye eneo moja la burudani jijini Entebbe Januari 22, 2018 na majeraha aliyopata yakasababisha damu kuganda kwenye ubongo, hali iliyosababisha afariki.

Share This Article