Mwanasiasa wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Moïse Katumbi, amepinga mapendekezo ya kufanyia katiba ya taifa hilo marekebisho.
Kiongozi huyo wa chama cha Together for the Republic, anasisitiza kwamba kinachostahili kupatiwa kipaumbele nchini DRC kwa sasa ni amani, hali ya kijamii na maendeleo ya miundombinu na wala sio mabadiliko ya katiba.
Akizungumza kuhusu mjadala unaoendelea, Katumbi alisema: “Tunayo Katiba nzuri sana. Unamaliza muhula wako wa miaka 5 au 10, kisha unaondoka. Kuna maisha baada ya siasa.”
Kauli hiyo inakuja wakati baadhi ya makundi ya kisiasa yanatoa hoja ya kufanya marekebisho ya Katiba, hatua ambayo imezua mjadala mkali ndani na nje ya nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Katumbi aliendelea kuonya vikali dhidi ya mpango huo akisema: “Wale wanaotaka kubadilisha Katiba watakuwa maadui wa watu wa Kongo na watabeba jukumu la kuigawa nchi yetu.”
Aidha, alisisitiza kuwa changamoto kuu zinazoikabili DRC kwa sasa zinahitaji kushughulikiwa haraka badala ya kuingia kwenye mjadala wa Katiba.
“Leo hii, tatizo si Katiba, bali ni amani, masuala ya kijamii na miundombinu,” aliongeza.
Katika tamko lake lenye lugha kali zaidi, Katumbi alihitimisha kwa kusema: “Kwa mtazamo wangu, kugusa Katiba ni jambo linalofanywa na watu ambao huenda wamepagawa na shetani, na watawajibika kwa hilo.”
Kauli hizi zinaongeza mvutano katika mjadala wa kisiasa nchini DRC, huku wachambuzi wakionya kuwa suala la mabadiliko ya Katiba linaweza kuwa chanzo cha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa endapo halitashughulikiwa kwa tahadhari.