Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa Mombasa

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati akamatwa Mombasa.

Maafisa wa Polisi wamewakamata washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarti katika  kaunti ya Mombasa.

Maafisa hao kutoka kitengo cha kukabiliana na mihadarati (ANU), walimtia nguvuni Tito Paul Mulu mwenye umri wa miaka 41 akiwa na kilo 250 za bangi katika eneo la Changamwe, huku mwenzake Oliver Ochieng mwenye umri wa miaka 23 akikamatwa katika eneo la Kisauni.

Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema baada ya kuhojiwa, Ochieng aliwapeleka maafisa hao kwenye nyumba yake ya kukodisha ambako walipata magunia mawili ya bangi.

Washukiwa hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani, huku bangi hiyo ikihifadhiwa kama ushahidi.

“Operesheni hii inaashiria kujitolea kwa kitengo cha ANU kuwatia nguvuni walanguzi wa mihadarati na kusambaratisha mitandao yao, kuhakikisha usalama wa jamii,” ilisema DCI.

Share This Article