Uganda kuandaa mkutano muhimu wa kidijitali Afrika

Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa Taifa nchini humo Chris Baryomunsi, alisema tukio hilo ni la Oktoba 6 hadi 8, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read
Chris Baryomunsi, Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa Taifa, Uganda 

Uganda imetangaza kuwa itakuwa mwenyeji wa toleo la mwaka 2026 la mkutano wa “Digital Government Africa”, jukwaa kubwa la bara linalolenga kuendeleza teknolojia katika sekta ya umma.

Katika mkutano na wanahabari, Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa Taifa, Chris Baryomunsi, alisema tukio hilo la Oktoba 6 hadi nane, litakutanisha viongozi wa serikali, watoa huduma za teknolojia, wawekezaji na washirika wa maendeleo kutoka kote Afrika na kwingineko.

Mkutano huo, utakaofanyika chini ya udhamini wa Serikali ya Uganda, utakuwa na kaulimbiu “Kuharakisha Mabadiliko ya Kidijitali ya Serikali Barani Afrika.”

Waziri Baryomunsi alisisitiza kuwa mageuzi ya kidijitali sasa ni msingi wa utoaji huduma, ukuaji wa uchumi na ushiriki wa wananchi, badala ya kuwa ndoto ya baadaye.

Alibainisha kuwa nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Uganda, zinawekeza katika mifumo kama utambulisho wa kidijitali, majukwaa ya serikali mtandaoni, usalama wa mtandao na malipo ya kidijitali ili kuboresha utawala wa umma.

Waziri huyo alieleza kuwa kuandaa mkutano huo ni hatua ya kimkakati na ya wakati mwafaka, akitaja maendeleo ya Uganda katika miundombinu ya TEHAMA, ubunifu na ujumuishaji wa kidijitali.

Aliongeza kuwa tukio hilo litaifanya Uganda kuwa kinara wa kikanda huku likifungua fursa za uwekezaji na ushirikiano.

DGA 2026 pia itajikita katika maeneo muhimu kama akili mnemba, ulinzi wa data na ujuzi wa kidijitali, huku ikihamasisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika zinazokabili changamoto zinazofanana.

Baryomunsi aliwataka wadau kote barani kushiriki, akisisitiza kuwa mkutano huo utasaidia kuunda mustakabali wa kidijitali wa Afrika kupitia maarifa ya pamoja na suluhisho za vitendo.

 

Share This Article