Rais wa Kenya William Ruto amesema Kenya na Tanzania zimetenga shilingi bilioni 130 za utekelezaji biashara na shilingi zingine bilioni 65 za uwekezaji wa mpakani.
Hata hivyo, Rais huyo ambaye yuko kwenye ziara ya kiserikai ya siku mbili nchini Tanzania, alisema ili hayo yaafikiwe ipo haja ya kuondoa vikwazo vinavyohujumu usafiri wa watu, mizigo na utoaji huduma.
“Biashara zitaimarika ikiwa vikwazo visivyo vya kodi vitaondolewa, vikiwemo ucheleweshaji wa mpakani, ukosefu wa usawa katika viwango vya ubora na upatikanaji wa soko,” alisema Rais Ruto.
Alisema serikali za nchi hizo mbili zimeweka muda wa hadi Juni 30, 2026 kuhakikisha vikwazo hivyo vyote vinaondolewa.
Akizungumza kwenye kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Kenya Jijini Dar es Salaam Jumatatu jioni, Ruto alisema mkutano huo utaandaliwa kila mwaka kuangazia hatua zilizopigwa na kutafuta fursa mpya.
Mkutano huo wa kibiashara uliwaleta pamoja wafanyabiashara zaidi ya 300, wakiwemo wale kutoka sekta kibinafsi.