Majaji wapya walioapishwa leo katika Ikulu ya Nairobi, wamehimizwa kufanya maamuzi ya busara na kusimama kidete kutetea maamuzi hayo watakapohitajika kufanya hivyo.
Ushauri huu ulitolewa na Rais William Ruto aliyeshuhudia uapisho huo, ambaye alitoa mfano wake mwenyewe akisema kwamba kamwe hajutii uamuzi wowote ambao amewahi kufanya kufikia sasa.
Kiongozi wa nchi alisema kwamba ana msimamo wa kutekeleza maamuzi magumu, ambayo mara nyingi hayapendelewi na wengi lakini yanalenga kusongesha nchi mbele, akihimiza majaji kufanya hivyo.
Alisisitiza kwamba kazi za majaji hao ni zaidi ya uteuzi na kuzembea kazini hakutaruhusiwa.
Majaji walioapishwa leo watahudumu katika Mahakama Kuu Nchini, Mahakama ya Mazingira na Ardhi na wengine 12 wakaapishwa kuhudumu katika Mahakama ya Haki ya COMESA.
Kati ya walioapishwa, 24 ni Mahakama Kuu na waliosalia 13 ni wa mahakama ya mazingira na ardhi.
Rais alijivunia hatua ya leo akisema majaji walioteuliwa katika muda katika ambao amekuwa madarakani sasa imefikia 98, akisisitiza kujitolea kwake katika kuhakikisha idara ya mahakama imewezeshwa na kufanikishwa.
“Katika kufanya hivyo, tunatekeleza sio tu ahadi yetu ya kuimarisha taasisi hii muhimu, bali pia kuimarisha jukumu lake kama nguzo kuu ya maendeleo jumuishi na Mlinzi wa imani ya umma katika utaratibu wetu wa kidemokrasia” alisema Rais.
Majaji wa COMESA wameapishwa nchini Kenya ikitizamiwa kwamba kwa sasa Kenya ndiyo inashikilia uenyekiti wa tume kuu ya COMESA kupitia kwa Rais Ruto.