Usiku wa Ijumaa Mei Mosi, 2026, ulikuwa wa kipekee katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, ambapo mkongwe wa muziki huo Profesa Jay alituzwa.
Hafla hiyo iliandaliwa katika viwanja vya 701 Kawe Garden na wakongwe wa Bongo Fleva Lady jaydee na Master Sugu pamoja na wengine kwa ajili ya kumuenzi Jay ambaye jina lake halisi ni Joseph Haule.
Tuzo hiyo ilitolewa kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya muziki nchini Tanzania na kuifanya kuwa ajira halisi kwa vijana, mchango ambao kwa miaka mingi umeweka msingi imara wa ukuaji wa tasnia ya burudani nchini humo.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, ambaye pia ni mwanamuziki mkongwe nchini tanzania, alitumbuiza kwenye hafla hiyo ishara ya jinsi viongozi wa serikali wanaweza kusimama na wasanii katika kukuza muziki.
Bongo Flava Honors ni jukwaa muhimu la utambuzi na la kihistoria linalounganisha kizazi kipya cha wasanii na nguzo zilizojenga tasnia ya muziki kwa miaka mingi nchini Tanzania.
Kando na heshima kwa Jay, hafla hiyo ilitumika pia kupitisha ujumbe kwa vijana wote kuwa muziki ni kazi, ni matumaini na ni dira ya mafanikio pale unapothaminiwa na kulindwa.
Wasanii ambao wamewahi kupokeza Bongo Fleva Honors ni pamoja na Master Sugu, Jay Moe, kundi la TMK Wanaume na Lady Jaydee.