Wakazi wa Kaunti ya Wajir waliandaa mkutano wa amani, unaolenga kukomesha mzozo wa kijamii katika mpaka wa Garissa na Kitui.
Mkutano huo ulioratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la Wajir Peace, uliwaleta pamoja wazee wa jamii, viongozi wa vijana pamoja na wadau mbalimbali, wakitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali za kiusalama ili kukabiliana na mizozo ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji wa ngamia.
Wito huo unajiri kufuatia machafuko yaliyoshuhudiwa na ambayo yalisababisha maafa akiwemo mvulana wa umri wa miaka 14 katika eneo la Ukasi Juma hili.
Mvulana huyo anadaiwa kuuawa na wafugaji wa ngamia, na kusababisha maandamano na kufungwa kwa barabara kuu ya Mwingi–Garissa kwa siku tatu.
Hali ya utulivu imerejea katika eneo la Mwingi baada ya serikali kuwapeleka maafisa wa usalama kudumisha amani.
Hata hivyo serikali imehimizwa kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kwenye mzozo huo.