Wamiliki Ngamia Kitui kusajiliwa ili kudumisha usalama

Tom Mathinji
2 Min Read
Wamili na wafugaji ngamia kaunti ya Kitui kusajiliwa.

Viongozi kutoka kaunti za Kitui na Garissa, wamependekeza hatua kali za kukabiliana na mizozo ya mpakani kati ya wakulima na wafugaji wa ngamia, ambayo imesababisha maafa kwa muda wa miaka kadhaa.

Kisa cha hivi karibuni kinahusisha mauaji ya mvulana wa umri wa miaka 14 mapema wiki hii na watu wanaoshukiwa kuwa wafugaji wa ngamia katika eneo la Ukasi, na kusababisha maandamano yaliyosababisha kufungwa kwa barabara kuu ya Mwingi – Garissa kwa siku tatu.

Pia, watu 7 waliuawa katika kijiji cha Kwa Kamari, Tseikuru na watu wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo.

Mashambulizi hayo yalisababisha kuandaliwa kwa mikutano ya pamoja ya kiusalama kati ya asasi za usalama na viongozi wa maeneo hayo kushughulikia changamoto hiyo ili kuepuka hasara zaidi.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyoratibiwa ni pamoja na kuwa na sajili ya wamiliki na wafugaji wa ngamia katika kaunti ya Kitui, huku sajili hiyo ikihifadhiwa na machifu na manaibu wao, na kisha kukabidhiwa kwa kamati za kiusalama za kaunti ndogo na kauti kwa tathmini zaidi.

Machifu hao watahitajika kufuatilia mienendo ya mifugo hao, hatua ambayo itarahisisha asasi za usalama kuzifuatilia na kuchukua htua za haraka iwapo kutakuwa na utovu wa usalama.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Gavana wa Kitui Dkt. Julius Malombe, alitoa wito kwa jamii zinazozozana kutogawanywa na wahalifu wachache waliokuwa wakitekeleza mauaji ya watu katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Gavana wa Garissa  Nathif Jama, alishutumu asasi za usalama kwa kuzembea kazini, akilalamika kuwa hadi sasa hawajamkamata yeyote kuhusiana na mauaji yaliyotokea katika eneo hilo.

“Ikiwa kuna wahalifu ambao wanawaua watu wetu, mbona hawajakamatwa? Hakuna haja ya swala kama hili kutokea na kisha tulalamike kama serikali,’ alishangaa Jama.

TAGGED:
Share This Article