IEBC yataja usajili uliohitimishwa kuwa uliofanikiwa

Wapiga kura wapya milioni 2.3 walisajiliwa huku lengo la awali likiwa milioni 2.5.

Marion Bosire
2 Min Read

Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu Mipaka Nchini, IEBC, imetaja awamu ya Kwanza ya mpango wa Usajili Endelevu Ulioboreshwa wa Usajili wa Wapiga Kura, ECVR, kuwa iliyofanikiwa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari leo, mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alitaja kuimarika kwa ufanisi na ongezeko kubwa la idadi ya wapiga kura waliosajiliwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa jijini Nairobi leo tarehe 30 Aprili 2026, Ethekon, alisema zoezi hilo lililofanyika kati ya tarehe 30 Machi na 28 Aprili, lilisajili jumla ya wapiga kura wapya milioni 2.3.

Ethekon alibainisha kuwa Tume ilianzisha zaidi ya vituo 30,000 vya usajili katika maeneo bunge yote 290, vikisaidiwa na maelfu ya maafisa na vifaa vya KIEMS, hatua iliyoboreshwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa huduma hiyo.

Usajili wa kila wiki ulizidi wapiga kura 500,000 baada ya wiki ya kwanza, hali iliyoashiria ongezeko kubwa ikilinganishwa na mazoezi ya awali ya usajili mwaka 2016 na 2021.

IEBC ilihusisha mafanikio hayo na mikakati muhimu kama mfumo wa “Open Kit” ulioruhusu wapiga kura kujisajili kutoka eneo lolote, upanuzi wa vituo vya usajili katika vyuo vikuu na vituo vya Huduma na upangaji unaotegemea takwimu katika kugawa rasilimali.

Licha ya mafanikio hayo, Tume ilikiri kuwepo kwa changamoto zikiwemo tofauti za kikanda, matatizo ya usafirishaji katika maeneo ya mbali, masuala ya usalama na kuenea kwa taarifa potovu.

IEBC ilisema usajili wa wapiga kura utaendelea huku maandalizi yakiongezwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 10 Agosti 2027, ikisisitiza umuhimu wa kuwa na daftari la wapiga kura lililo sahihi na jumuishi.

Share This Article