Mama Taifa Bi. Rachel Ruto hii leo amezindua mradi wa maji alioahidi awali katika shule ya Unoa iliyoko huko Wote, kaunti ya Makueni.
Mkewe Rais alisema kwamba alirejea katika taasisi hiyo ya masomo ambayo alizuru Juni 16, 2025 kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kuzindua mradi huo alioahidi wakati huo.
“Nilirejea shuleni Unoa Wote, kaunti ya Makueni, ambapo ahadi niliyotoa wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, sasa ni mabadiliko yaliyotimia,” aliandika Bi Rachel.
Kulingana naye, eneo la shule hiyo lililokuwa limejaa vumbi, sasa ni eneo la hadhi na mazingira mema kwa ajili ya masomo, likiwa na maji kutoka kwa kisima kilichochimbwa hivi maajuzi.
Alisema pia kwamba viwanja vya shule hiyo sasa ni vya kijani, madarasa yamekarabatiwa na shamba la mboga na matunda lipo kwa ajili ya masomo na kwa ajili ya matumizi.
Mama Rachel alisema kwamba aliafikia ufanisi huo shuleni Unoa kwa ushirikiano na Wizara ya maji na ile ya mawasiliano na uchumi dijitali, ambapo aliweza pia kuipa shule hiyo vifaa vya kidijitali.
Alitaja pia jamii ya Dawoodi Bohras, ambayo pia ilichangia ufanisi huo akisema, “Tunaona kinachowezekana wakati uongozi unasikiliza, jamii zinachukua hatua na washirika wanajibu”.
Mama taifa alikuwa na zawadi nyingine kwa ajili ya kila mwanafunzi ile ya viatu na soksi, kama njia ya kuhakikisha wanatembea safari ya elimu wakijihisi wenye hadhi.