Israel Mbonyi kuandaa tamasha Uingereza mwezi Juni

Ziara hiyo imezua hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu ziara yake ya awali iliyopangwa kufanyika kote nchini Rwanda.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili wa asili ya Rwanda Israel Mbonyi, amethibitisha kwamba ataandaa tamasha mjini Leeds, Uingereza, tarehe 27 Juni mwaka huu kama sehemu ya ziara yake ijayo ya kimataifa.

Mbonyi pia anatarajiwa kutumbuiza mjini Braunschweig, nchini Ujerumani, tarehe 20 Juni mwaka huu wa 2026, ingawa bado halijatangazwa rasmi.

Maonyesho hayo mawili ni sehemu ya ziara yake ya majira ya joto barani Ulaya na maeneo mengine ya kimataifa, huku akiendelea kupanua huduma yake nje ya Rwanda.

Ratiba hii mpya imekuja wakati kukiwa na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu ziara yake ya awali iliyopangwa kufanyika kote nchini Rwanda.

Mbonyi anaripotiwa kuelelekeza nguvu zake kwenye ziara ya Ulaya baada yake na waandaaji wa ndani, Ma Africa, kukubaliana kufuta ziara ya ndani kwa sababu ambazo bado hazijafichuliwa.

“Muda huu tumejikita katika shughuli nyingine. Sina mengi ya kusema kuhusu ziara ya nchini,” alisema mmoja wa waandaaji.

Aliongeza kusema kwamba kulikuwa na mpango wa kupeleka matamasha kote nchini Rwanda mwaka huu, lakini wakagundua mambo ambayo sio ya faida kwao.

Matamasha yajayo ni sehemu ya mpango mpana wa kutangaza albamu yake ya hivi karibuni, Hobe, ambayo aliizindua wakati wa tamasha la kurekodi moja kwa moja katika Ukumbi wa Intare Oktoba 2025.

Hobe, albamu ya sita ya Mbonyi studio, ina nyimbo 14 zilizoimbwa kwa Kinyarwanda, Kiingereza na Kiswahili. Mradi huo unachanganya mitindo mbalimbali ikiwemo Amapiano, Afrobeats, soul, na Gakondo—ukiunganisha ladha za jadi na sauti za kisasa za injili.

Mbonyi ameendelea kuwa na mwelekeo thabiti wa ubunifu tangu albamu yake ya kwanza Number One mwaka 2014. Orodha ya kazi zake pia inajumuisha Intashyo (2017), Mbwira (2020), Hari Ubuzima (Live) (2022), Umusirikare (2023), na Hobe (2025).

Share This Article