Waziri wa Usalama wa Taifa wa Kenya Kipchumba Murkomen, amewapongeza maafisa wa polisi wa Kenya wanaohudumu chini ya kikosi cha kimataifa cha kudumisha amani nchini Haiti (MSS), huku muda wao wa kuhudumu ukikaribia kukamilika.
Akizungumza Jumatatu alipotembelea maafisa hao waliosalia nchini Haiti, Murkomen aliwapongeza maafisa hao kwa kujitolea mhanga kudumisha amani na uzingatiaji Sheria katika taifa hilo.
Murkomen na ujumbe wa Kenya walilakiwa nchini Haiti na kamanda wa kikosi cha MSS Godfrey Otunge, na afisa wa ubalozi wa Kenya nchini Haiti Noor Gabow, miongoni mwa maafisa wengine.
Akiwahutubia maafisa hao, Waziri huyo aliwapa ujumbe wa heri njema kutoka kwa Rais William Ruto na watu wa Kenya kutokana na jukumu lao la kupigiwa mfano.
“Maafisa wetu chini ya kikosi cha MSS, walihudumu kwa kujitolea na walipandisha bendera ya Kenya juu zaidi,” alisema Murkomen
Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliwapongeza maafisa hao wa polisi kwa kutekeleza majukumu yao kwa utaalam, nidhamu na maadili, akishukuru washirika wa kimataifa kwa kupiga jeki MSS.
Aliwahimiza maafisa hao wanorejea nchini Kenya, kutumia tajiriba waliopata wakiwa katika kikosi hicho, kuwahudumia watu wa Kenya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mshauri wa Taifa kuhusu Usalama Joseph Boinett, alisema maafisa hao walihudumu kwa nidhamu na uadilifu wa hali juu na kujitolea.
Alitaja operesheni hiyo kuwa ya kihistoria, akidokeza maafisa hao walishikilia sifa ya Kenya kwa heshima huku wakuchangia kuleta amani na uthabiti katika nchi ya kigeni.