Bunge la Taifa lapunguza Ushuru Ziada wa Thamani kwa bidhaa za Petroli

Tom Mathinji
2 Min Read
Kikao cha Bunge la Taifa.

Bunge la Taifa siku ya Alhamisi limeidhinisha Mswada wa marekebisho wa Ushuru Ziada wa Thamani (VAT) wa mwaka 2026, unaopunguza Ushuru Ziada wa Thamani-VAT kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8.

Hatua  hiyo inayolenga kudhibiti gharama ya juu ya mafuta, licha ya misukosuko ya bei za mafuta inayoshuhudiwa kimataifa.

Akiwasilisha Mswada huo, Naibu Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Owen Baya, alihusisha ongezeko la bei za mafuta na changamoto zinazoshuhudiwa Mashariki ya Kati, ambazo zimesababisha usambazaji wa bidhaa hiyo muhimu.

“Vita ambavyo vinamekuwa vikishuhudiwa Mashariki ya Kati, vimeathiri taifa hili. Sio sera za hapa nchini ambazoo zimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta, lakini misukosuko ya kimataifa,” alisema Baya.

Wakijadili mswada huo, wabunge walielezea mswada huo kuwa hatua ya dharura kwa lengo la kuwakinga wakenya kutokana na ongezeko la bei ya mafuta.

Walisema mswada huo ni muhimu ili kuruhusu marekebisho ya ushuru kwa zaidi ya asilimia 25 ya kiwango kinachoruhusiwa kwa waziri wa fedha kubadilisha ushuru ziada wa thamani chini ya masharti yaliyopo.

Kupunguzwa kwa ushuru huo kutatekelezwa kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa muda wa siku 90.

Mswada huo utasababisha mafuta ya Petroli kuuzwa shilingi 197.60, Dizeli shilingi 206 na Mafuta Taa shilingi 196.63 na hivyo kutoa afueni ya muda kwa wakenya utakapotiwa saini.

TAGGED:
Share This Article